Eneo la MNK Fuvu (Mary Nicol Korongo, MNK) lipo katika upande wa pembeni wa bonde la Olduvai, na ni moja ya eneo muhimu zaidi la kiakiolojia katika bonde la Olduvai, kwasababu Mary Leakey aligundua mabaki ya zamadamu katika eneo hilo (OH 13, OH 14, na OH 15) ambayo yalitumika kama utambulishi wa zamadamu anaitwa Homo habilis.
Mfupa wa taya wa Cinderella (OH13), uliyogunduliwa na Mary Leakey miaka ya 1960, ndie kielelezo cha zamadamu wote wa aina ya Homo habilis.
Zamadamu mwenye namba OH 13 (ambae pia jina lake la utani ni Cindy, au Cinderella) ndie kielelezo cha zamadamu wote wa aina ya Homo habilis. Mabaki yake yaliyo gunduliwa ni sehemu ya juu ya fuvu, taya, pamoja na mifupa na meno ya juu na chini.
Makusanyo muhimu ya kiakiolojia yaligunduliwa katika usawa huohuo wa mabaki ya zamadamu, yakijumuisha ushahidi wa mwisho wa mabaki ya Homo habilis kwenye matabaka ya bonde la Olduvai, pamoja na zana za mawe ambazo hazina handaksi.
Uchimbaji wetu kwenye kwenye eneo hilo kati ya mwaka 2010 na 2014, ndio ulikuwa wa kwanza kufanywa tangu kazi za awali za wakina Leakey katika miaka ya 1960, na ulilenga kuboresha muktadha wa kiakiolojia ambapo mabaki ya Homo habilis yaligunduliwa.
Sehemu za machimbo katika eneo la MNK Fuvu.
Matokeo ya upimaji wa kiwango cha muda uliopita kwa kutumia matabaka, yanaonyesha kuwa eneo la MNK Fuvu lipo katikati ya tabaka la kijiolojia la II, chini ya tabaka la IIB. Makusanyo yaliletwa na kuwekwa na maji karibu na ufukwe wa ziwa katika kipindi cha muda mrefu, tofauti na dhana ya awali kuwa makusanyo hayo yalitokana na eneo hilo kuwa makazi ya zamadamu.
Mwanzo wa upanuzi uliofanywa na OGAP wa mashimo ya machimbo ya wakina Leakey yalioko upande wa kusini.
Mtazamo wa jumla wa shimo la machimbo la T36.
Mashimo ya machimbo ya OGAP-T3 baada ya kukamilika kwa uchimbaji.
Sehemu kuu ya kiakiolojia katika T36 kutoka juu ya shimo la machimbo.
Makusanyo ya zana za mawe yametawaliwa na teknolojia ya core na flake ambapo kupiga kwa kutumia mikono huru kipindi cha utenegenezaji hutawala. Uwiano wa makundi ya kiteknolojia na vipengele vya teknolojia vya makusanyo haya, vinayapa sifa makusanyo haya ya MNK Fuvu kuwa katika kundi la tekinolojia ya Oldowan.
Kipande cha jiwe la kawaida kilichohusishwa kwasababu ya ukaribu wake, kikiwa pamoja na kipande cha kisukuku katika sehemu kuu ya kiakiolojia ya shimo la machimbo namba T3 ndani ya eneo la MNK Fuvu.
Flake ya aina ya chert ikionekana kwa wima wakati wa uchimbaji wa eneo kuu.
Core ya malighafi ya phonolite kutoka sehemu kuu ya kiakiolojia katika shimo la machimbo la T3 – MNK Fuvu.
MNK Fuvu ndio eneo la mwisho lenye mabaki yasiokuwa na handaksi pale Olduvai, na hivyo kuwa alama inayoashiria mwisho wa tknolojia ya Oldowan katika bonde la Olduvai. Kwahivyo, likiwa na umri wa takriban miaka millioni 1.67, eneo la MNK Fuvu ni muhimu katika kuelewa mwisho wa teknolojia ya Oldowan na namna Homo habilis alivyotoweka Afrika mashariki.